Friday, March 14, 2014
Sudan yaitaka UN kuwaadhibu waasi wa Darfur
Serikali ya Sudan imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuyaadhibu makundi ya waasi ambayo yanafanya mashambulizi dhidi ya maslahi ya serikali katika jimbo la Darfur la magharibi mwa nchi hiyo. Hassan Hamid, naibu balozi mdogo wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, ameyasema hayo kupitia ujumbe aliouwasilisha kwa uongozi wa baraza hilo akilalamikia mashambulizi ya waasi katika baadhi ya maeneo ya Darfur. Katika ujumbe huo Hassan Hamid ameashiria kwamba, makundi ya waasi yanapinga mwenendo wa amani kupitia mashambulizi yao dhidi ya maeneo na vijiji vya jimbo hilo, na kuongeza kuwa, hatua kama hizo zinachochewa na moja kwa moja hatua ya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Sudan (SPLA) tawi la kaskazini mwa Sudan, ambayo jeuri na kiburi chake, kimepelekea kuvunjika kwa mazungumzo ya kusaka amani kati yake na serikali huko mjini Addis Ababa, Ethiopia. Akiashiria kukosekana wanajeshi wa serikali wa kulinda amani katika maeneo hayo na kuzuia mashambulizi ya waasi, Hamid amesema, makundi ya waasi yanatumia fursa hiyo kuwashambulia raia na kufanya jinai nyenginezo pamoja na kuharibu miundombinu nchini Sudan. Hayo yanajiri katika hali ambayo jana Makamu wa Rais wa Sudan Hassabo Mohammed Abdul Rahman, alinukuliwa akisema kuwa nchi yake imejiandaa kikamilifu kupambana na kuyafyeka makundi ya waasi katika eneo hilo la Darfur, la magharibi mwa nchi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment