Saturday, March 15, 2014
Naibu mkuu wa Jab'hatu Nusra auawa Yabrud, Syria
Jeshi la Syria limeingia katika mji wa al Qalamun huko Yabrud katika mapambano ya kuusafisha na makundi ya kigaidi huku taarifa za uhakika zikisema kuwa, naibu mkuu wa kundi la kigaidi la Jab'hatu Nusra nchini Syria, Abu Izam al-Kuwaiti, ameuliwa na jeshi la Syria katika mji huo.
Gaidi huyo ndiye aliyekuwa msimamizi wa faili la ubadilishanaji wa watawa wa Kikristo wa mji wa Ma'loula ambao miezi minne iliyopita walitekwa nyara na kundi hilo la Jab'hatu Nusra na kuwapeleka mjini Yabrud.
Tayari kundi hilo la kitakfiri, limethibitisha katika mtandao wa kijamii wa Twitter habari ya kuuawa kiongozi wake huyo. Mji wa Yabrud, unahesabiwa kuwa ni ngome kuu na muhimu zaidi ya makundi ya kitakfiri yanayoendesha ukatili, mauaji na uharibifu nchini Syria.
Wanamgambo wengi wa kundi la kigaidi wa Liwau Ahrar al-Qalamun wameukimbia kutoka mji wa Yabrud baada ya jeshi la Syria kuanzisha operesheni ya kuusafisha mji huo. Habari zaidi zinasema kuwa, wanamgambo kadhaa wa kundi la Jab'hatu Islamiyyah wameuliwa na magaidi wenzao wa kundi la Jab'hatu Nusra wakati walipokuwa wakikimbia kutoka mjini humo.
Jeshi la Syria lilianza kuingia katika mji huo hapo jana baada ya kuwashinda wanamgambo wa Jab'hatu Nusra katika maeneo ya mashariki na kaskazini na kisha kufunga haraka njia za kuingia na kutoka mjini humo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment