Pages

zaman leo

Jumatatu, Machi17, 2014



Leo ni Jumatatu tarehe 15 Mfunguo Nane, Jamadil Awwal mwaka 1435 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 17 Machi mwaka 2014 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1397 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali sala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

 Miaka 19 iliyopita kama leo, alifariki dunia Sayyid Ahmad Khomeini mwana wa kiume wa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini M.A. Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya na akapata malezi na elimu kutoka kwa baba yake. Hujjatul Islam Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuanzisha mawasiliano na kuwa kiunganishi kati ya Imam Khomeini M.A na wanamapinduzi.

Na miaka 1378 iliyopita inayosadiafina na leo, ardhi ya Baitul Muqaddas huko Palestina ilikombolewa na Waislamu. Vita vya kwanza kati ya Waislamu na Warumi vilijiri huko kaskazini mwa Bahari Nyekundu baada ya kudhihiri Uislamu. Jeshi la Waislamu lilitoa pigo kwa Warumi na eneo la kusini mwa Palestina likakombolewa katika zama za utawala wa Umar bin Khattab. Baada ya kushindwa huko, mfalme wa Roma alituma jeshi kubwa katika ardhi za Palestina. Warumi walishindwa vibaya na jeshi la Kiislamu katika vita vilivyojiri huko Palestina na mwishoni mwa mapigano hayo, kamanda wa jeshi la Roma aliuawa na Damascus ikadhibitiwa na Waislamu

No comments:

Post a Comment