Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya amesisitiza kuwa, nchi yake iko pamoja kwa hali na mali na ndugu zao wa Palestina. Mohammad Abdulaziz ameyasema hayo katika kikao cha pamoja cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kamisheni ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuchunguza haki zisizokanushika za wananchi wa Palestina, kilichofanyika mjini Cairo, Misri na kusisitiza kuwa, kamwe Libya haitabadili msimamo wake katika kuhakikisha wananchi wa Palestina wanapatiwa haki zao za kimsingi ikiwemo kuundwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baitul Muqaddas. Abdulaziz ameongeza kuwa, kikao hicho kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, kilikuwa na malengo ya aina moja, ambayo ni kuutangaza mwaka huu wa 2014 kuwa mwaka wa kuwasaidia na kushirikiana na wananchi madhlumu wa Palestina. Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya amesema kuwa, tayari kumefanywa juhudi kadhaa kwa ajili ya kuvutia uungaji mkono wa jamii ya kimataifa kwa wananchi wa Palestina. Kwa upande mwingine, Abdulaziz amesisitizia udharura wa kutatuliwa kadhia ya Palestina kwa msingi wa azimio nambari 194 la Baraza la Usalama. Azimio hilo linasisitiza juu ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina sambamba na kulipwa fidia.
No comments:
Post a Comment