Jumapili, Machi 16, 2014
Leo ni Jumapili tarehe 14 Mfungo Nane Jamadul-Awwal mwaka 1435 Hijria, inayosadifiana na tarehe 16 mwezi Machi 2014 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, utawala wa Baath nchini Iraq uliushambulia bila huruma na kwa mabomu ya kemikali za sumu mji wa Halabcha wa wakazi wa Kikurdi huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwa kutumia makumi ya ndege za kivita. Hujuma hiyo ilianza baada ya kushindwa kupambana na wapiganaji Waislamu wa Iran na wa Kikurdi wa huko Iraq, na katika upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabcha waliwakaribisha wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo wa Saddam Hussein dhidi yao. Raia elfu tano wasio na hatia waliuawa kutokana na kuvuta gesi ya sumu huko Halabcha. Hata hivyo nchi za Magharibi hazikuchukua hatua yoyote mbele ya jinai hiyo kubwa na ya kutisha.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Selma alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika fani ya fasihi mwaka 1909.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, kikosi cha Red Brigade kilimteka nyara Aldo Moro Waziri Mkuu wa zamani wa Italia. Moro alikuwa mfuasi wa chama cha Kidemokrasia cha Kikristo cha Italia na kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa duru tano. Wanachama 65 wa Brigedi Nyekundu walimuuwa mwanasiasa huyo baada ya kumteka nyara. Brigedi Nyekundu lilikuwa kundi la mrengo wa kushoto lenye misimamo ya kufurutu ada huko nchini Italia lililokuwa likiitaka nchi hiyo kuachana na taasisi za Magharibi khususan Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi NATO.
Na siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, alifariki dunia mjini Tehran dunia Haj Mulla Ismail Sabzawari, mpokezi wa hadithi na hatibu mkubwa wa karne ya 13 Hijria. Mulla Sabzawari alizaliwa katika eneo la Sabzawar lililoko kaskazini mashariki mwa Iran. Alijifunza falsafa kwa Mulla Hadi Sabzawari aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya Mwanafalsafa wa Mashariki. Baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu zaidi na kupata daraja ya ijtihad. Msomi huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Majmaun Nurain" na "Nawadirul Athar".
No comments:
Post a Comment