Pages

Monday, March 17, 2014

Dawa za Kurefusha Maisha ya Waathirika wa Ukimwi ARV


 

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na mko tayari kando ya redio zenu ili kufuatilia sehemu nyingine ya mfululizo wa makala za kipindi cha Ijue Afya Yako. Leo nitazungumzia juu ya dawa za kurefusha maisha ya waathirika wa ukimwi yaani ARV, lengo likiwa ni kuongeza ufahamu kuhusiana na matibabu ya ugonjwa huu hatari. Karibuni muwe nami hadi mwisho wa kipindi.

&&&&&&

Sote tunatambua kuwa hadi sasa ugonjwa hatari wa Ukimwi ambao ni tishio kwa dunia kwa kuwa unasababisha vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka hauna kinga wala tiba mujarabu. Hata hivyo kuna dawa ambazo huweza kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi na hivyo kusaidia kupunguza madhara ya vijidudu hivyo katika mfumo wa kulinda mwili. Dawa hizo huitwa antiretrovirals kwa kifupi ARV's na matibabu yake hujilikana kama Antiretroviral Therapy. Dawa hizi hupambana na virusi vinavyosababisha Ukimwi na kuwasaidia wale walio na virusi hivyo kuwa na afya nzuri. ARV hupunguza kasi ya kuzaliana virusi vya HIV na wakati virusi hivyo vinapozaliana kwa kasi ndogo huwa na uwezo mdogo wa kuathiri mfumo wa ulinzi wa mwili. Iwapo mfumo wa kulinda mwili unafanya kazi vyema, uwezekano wa mwili kupatwa na magonjwa hupungua. Mfumo wa ulinzi wa kila mtu ndio kinga inayozuia mwili kushambuliwa na maradhi, na kwa ajili hiyo kwa kuwa dawa za ARV hupunguza madhara ya virusi  vya HIV ya kuuharibu mfumo wa kulinda mwili, iwapo dawa hizo zitatumiwa kama ipaswavyo, huweza kumsaidia mgonjwa wa Ukimwi kuishi maisha marefu na kuwa na afya nzuri. Kabla ya kusonga mbele na kipindi chetu ni bora tuyajue malengo ya matibabu ya dawa za ARV's kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi:

1.      Kuhakikisha kwamba virusi vya HIV vinadhibitiwa kwa kiasi kikubwa katika mwili wa muathiriwa kwa kuvizuia visizaliane zaidi.

2.      Kuhuisha na kulinda utendaji kazi wa kinga za mwili kwa kuzijaza upya seli za CD4.

3.      Kupunguza vifo na magonjwa yanayoambatana na virusi vya HIV.

4.      Kwa muda mrefu kuboresha maisha ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi. 

&&&&&&

Lakini je, dawa za kurefusha maisha ya waathirika wa Ukimwi yaani ARV zinafanya vipi kazi mwilini? Ili kujibu swali hilo inabidi kwanza tujue hatua anwai za maisha ya kirusi cha HIV mwilini au lifecycle ya kirusi hicho. HIV huathiri seli za mfumo wa kulinda mwili na kuzigeuza seli hizo kuwa kama kiwanda cha kutengeneza virusi hivyo, kwani kirusi kimoja cha Ukimwi huweza kujigawanya na kutengeneza mamilioni ya virusi kama hivyo kwa kutumia seli za mwili wa muathiriwa. Seli zinaolengwa na kutumiwa na HIV ni seli zinazoitwa CD4, ambazo ni sehemu muhimu ya mfumo wa kulinda mwili. Baada ya virusi vya HIV kuingia katika seli hizo hupitia hatua kadhaa kabla virusi vingine vya HIV havijaanza kuzaliwa. Aina tofauti za dawa za ARV hutumika kusaidia katika steji tofauti za mzunguko wa maisha ya virusi vya HIV mwilini.

Ili matibabu ya dawa za ARV yaweza kuleta athari inayotakiwa kwa muda mrefu, inabidi mgonjwa wa Ukimwi atumie au ameze zaidi ya aina moja ya dawa hizo. Tiba hiyo huitwa tiba mseto na humaanisha kutumia dawa mchanganyiko za ARV katika matibabu ya Ukimwi. Takwimu zinaonyesha kuwa, watu wengi waliotumia dawa mchanganyiko walipata nafuu ikilinganishwa na wale waliotumia dawa aina moja.  Kwa mfano  kuna watu ambao walikuwa wameshindwa  hata kuendelea na shughuli zao za kila siku kutokana na kudhoofika na ugonjwa wa Ukimwi, lakini baada ya kutumia dawa hizo wameweza kurudi katika hali zao za kawaida na kuendelea na shughuli zao mbalimbali maishani. Pia ili tiba hiyo ifanikiwe mgonjwa wa Ukimwi anapaswa kufuata maelekezo ya daktari au mhudumu wa afya kuhusiana na namna ya kumeza dawa za ARV kama inavyotakiwa. Katika matibabu ya Ukimwi kwa kutumia madawa mchanganyiko au Combination Therapy, kwa kawaida aina tatu za dawa hizo hutumika ili kuwasaidia watu wenye Ukimwi, na aina hizo tofauti za dawa hupigana na virusi kwa njia tofauti, ili kuleta mafanikio zaidi katika kupambana na virusi vya HIV. Kwa kawaida kuna mchanganyiko wa aina tofauti, lakini baadhi ya dawa hizo hawa haziwezi kutumiwa kwa pamoja kwani, hufanya kazi kinyume cha dawa nyingine. Pia dawa hizi za ARV kwa kiasi fulani huweza kutumiwa na watoto walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi.

&&&&&&&&

Wasikilizaji wapenzi mnategea sikio Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kipindi kilichopo hewani ni cha Ijue Afya Yako. Matibabu mengine kwa wagonjwa wa Ukimwi ni ya kutumia aina moja ya dawa au Monotherapy. Katika matibabu haya dawa aina moja tu hutumika ambapo lengo ni kupunguza hatari ya kuambukiza virusi vya Ukimwi. Kwa mfano kumzuia mama mjamzito asimuambukize mtoto wake tumboni. Tiba ya aina hii haitumiwi sana kwa sababu, mwili hujenga kinga dhidi ya aina moja ya dawa baada ya muda fulani. Matumizi ya dawa za ARV yanaweza kuwa njia ya kuzuia kuenea kwa Ukimwi kwa njia mbili. Mosi ni kwa kuwatibu watu wenye virusi vya Ukimwi walioingia kwenye hatari ya kuingia katika stegi ya Ukimwi na kushambuliwa na magonjwa mbalimbali na pili ni kuwapa nafuu watu walio na virusi ili kuzuia maambukizo zaidi ya ugonjwa huo.

Wasikilizaji wapenzi kama tunavyojua ugonjwa wa Ukimwi hauna tiba mujarabu ambayo inaweza kuviteketeza kikamilifu virusi vya HIV katika mwili wa muathirika, na ijapokuwa kuna dawa za kurefusha maisha ya waathirika wa Ukimwi lakini bado ugonjwa huu ni changamoto kubwa kwa afya ya mwanadamu. Ni vyema tukumbuke kuwa, watu wengi wanaendelea kuambukizwa virusi vya Ukimwi duniani na kwa kiasi kikubwa barani Afrika hasa katika eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara, huku kwa bahati mbaya, nusu ya maambukizo hayo yakiwakumba watu wasio na uwezo wa kununua dawa hizo pamoja na kushindwa kuzitumia ipasavyo. Nukta ya kuzingatia kuhusiana na dawa za ARV ni kuwa, matumizi ya dawa hizi za kuwaongezea maisha waathirika wa Ukimwi yanahitaji mgonjwa kula chakula bora wakati amapomeza dawa hizi. Mgonjwa pia anapaswa kunywa maji mengi na kuhakikisha kwamba anahifadhi dawa hizi katika mazingira mazuri. Vilevile dawa hizi hutumiwa na wale walioambukizwa virusi vya HIV baada ya kupima na kushauriwa kitaalamu hospitalilini au kwenye vituo vya afya kuanza kutumia dawa hizo kulingana na namna walivyoathirika. Kwa kawaida matumizi ya dawa za ARV hayaanzi baada tu ya mtu kuathirika na virusi vya Ukimwi, bali pale seli za CD4 zinapofikia 350 au pale muathirika wa HIV anapoingia katika hali ya Ukimwi ambayo ni pale mtu anapopata magonjwa nyemelezi yanayoambatana na ugonjwa huo. Pia mgonjwa wa Ukimwi anapaswa kupata ushauri maalumu ili kumtayarisha na matibabu ya ARV kabla ya kuanza kutumia dawa hizo. Imeonekana kuwa mgonjwa anaweza kuzoea kwa urahisi kutumia dawa hizi, lakini pia imeshuhudiwa kuwa matibabu haya baadhi ya wakati huwa magumu hasa kwa wagonjwa wenye hali duni za maisha. Hofu ya kudhulumiwa, kuchukiwa, kutengwa na kubaguliwa yote hayo huwafanya baadhi ya wagonjwa wengi wa Ukimwi barani Afrika kukataa kutumia dawa hizi za ARV.

&&&&&&

Ijapokuwa dawa za ARV haziwezi kuutibu kikamilifu ugonjwa wa Ukimwi na kumfanya mgonjwa asiwe tena na virusi hivyo lakini matumizi ya dawa hizo yana faida kubwa kwa wagonjwa wa Ukimwi. Hasa kwa kuwa huuhuisha na kulinda mfumo wa ulinzi wa mwili, hudibiti na hupunguza kasi ya kuzaliana virusi na kwa ujumla kuboresha maisha ya mgonjwa wa Ukimwi na mwishowe kumrefushia umri. Dawa hizo pia zinaweza kumletea madhara mtumiaji kama vile kuharisha, uchovu, maumivu ya kichwa na kadhalika hata kama zitatumiwa kama inavyotakiwa. Suala hili halimaanishi kuwa dawa hizo hazifai kutumiwa la hasha! Bali faida zake ni kubwa zaidi kuliko madhara yake. Iwapo hali hiyo itatokea, wanaotumia dawa hizi wanashauriwa kujadili suala hilo na daktari husika ili waweze kusaidiwa kupunguza madhara hayo. Pia wagonjwa wanashauriwa kupata ushauri wa daktari kabla ya kufanya mabadiko yoyote katika matumizi ya dawa za ARV.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, tangu ulipotambulika ugonjwa wa Ukimwi umesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 30 hadi mwaka 2009 na inakadiriwa kuwa, watu zaidi ya milioni 34 wanaishi na virusi vya HIV duniani. Licha ya kuwa bado hakuna dawa mujarabu ya kutibu Ukimwi lakini tunaweza kujiepusha kupata ugonjwa huu ikiwa tutazingatia njia tofauti za kujikinga na hasa kujiepusha na uasherati.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

No comments:

Post a Comment