Pages

Monday, March 17, 2014

Russia yatumia kura ya turufu kuhusu Crimea


 

Rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa iliyokuwa na lengo la kupinga kura ya maoni inayofanyika kwenye jimbo linalojitawala la Crimea huko Ukraine imegonga mwamba baada ya Russia kutumia kura yake turufu kuipinga huku China ikiepuka kupendelea upande wowote ambapo wajumbe 13 waliunga mkono. Kwa mujibu wa kanuni za Baraza la Usalama kura turufu ina uwezo wa kuzuia kupita kwa azimio lolote la baraza hata kama wajumbe wengi wataunga mkono. Baraza hilo lina wajumbe watano wenye kura turufu ambao ni China, Ufaransa, Uingereza, Russia na Marekani. Kura ya maoni Crimea inafanyika leo tarehe 16 kuamua iwapo jimbo hilo lijitenge na Ukraine na kujiunga na Russia. Rasimu hiyo iliyopigiwa kura jana ilikuwa inasema inazingatia umoja, utaifa na mamlaka ya Ukraine.

Akizungumza baada ya azimio hilo mwakilishi wa kudumu wa Russia  Balozi Vitaly Churkin amesema serikali yake itaheshimu uamuzi wa Crimea. Mgogoro kati ya Wamagharibi na Russia kuhusu Ukraine ulianza mapema mwezi huu, baada ya Moscow kuamua kupeleka vikosi vyake katika eneo lenye utawala wa ndani la Crimea, ikiwa ni baada ya Bunge la Ukraine kumuuzulu Rais Viktor Yanukovych aliyekataa kusaini makubaliano ya kibiashara na Umoja wa Ulaya. Bunge hilo lilimteua mwanasiasa muitifaki wa nchi za Magharibi Oleksandr Turchynov kuwa rais wa muda. Punde baada ya uamuzi huo Bunge la Crimea lilitaka kuitishwa kura ya maoni ya kuamua iwapo eneo hilo liwe sehemu ya Russia au Ukraine.

No comments:

Post a Comment