Dakta Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran asubuhi ya siku ya Jumatano alianza safari yake ya kwanza katika nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi kwa kuitembelea Oman ili kuanzisha awamu mpya ya uhusiano wa jadi na wa karibu uliopo baina ya nchi mbili. Safari hiyo ilifanyika katika hali ambayo Sultan Qaboos bin Said wa Oman alikuwa kiongozi wa kwanza wa nje kufanya safari hapa nchini kwa madhumuni ya kuja kumpongeza Dakta Hassan Rouhani kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Safari ambayo iliendeleza uhusiano wa kirafiki wa miaka na miaka baina ya nchi mbili na kuonyesha pia hamu ya Oman ya kuimarisha na kustawisha zaidi uhusiano wake na Iran.
Katika miezi iliyopita pia nchi hizi mbili zimeshuhudia safari za viongozi wa pande mbili pamoja na ahadi na makubaliano kadhaa yaliyofikiwa ambayo yameonyesha matumaini ya mustakabali mzuri wa uhusiano wa karibu uliopo baina ya nchi mbili, kiasi kwamba Oman sasa inatajwa kuwa mshirika nambari moja na wa kuaminika wa Iran katika eneo.
Kwa sababu hiyo kuanza safari ya kieneo ya Rais Rouhani huko nchini Oman lilikuwa jambo la kutarajiwa na hasa ikizingatiwa kwamba mazingira ya maelewano na makubaliano baina ya nchi mbili katika nyanja mbalimbali yalikuwa yameshaandaliwa kitambo nyuma.
Kuwemo Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mafuta, Kazi na Masuala ya Kijamii, Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Utalii, Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Mazingira na Gavana wa Benki Kuu katika msafara wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulioelekea nchini Oman kwa safari rasmi ya siku mbili kumedhihirisha umuhimu na upana wa masuala yaliyopangwa kujadiliwa na kufikiwa makubaliano baina ya nchi mbili.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Jumatano hiyohiyo kati ya Rais Rouhani na Sultan Qaboos, viongozi hao walitilia mkazo kustawishwa ushirikiano baina ya nchi mbili katika nyanja zote. Aidha mbali na kukubaliana kuhusu utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika safari ya mwezi Agosti mwaka jana aliyofanya Mfalme wa Oman hapa nchini walieleza matumaini yao pia kwamba uhusiano wa Iran na Oman utaweza kuwa mfano wa kustawisha uhusiano baina ya nchi za eneo hili la Ghuba ya Uajemi.
Kwa kuzingatia fursa na mazingira ya utangulizi yaliyopo, nchi mbili za Iran na Oman zimekubaliana kustawisha zaidi ushirikiano wao katika sekta za nishati, vyombo vya baharini, ushuru wa forodha, masuala ya fedha, hifadhi ya mazingira, utalii pamoja na ushirikiano wa kisayansi, utafiti na vyuo vikuu.
Katika safari ya siku mbili ya Rais Hassan Rouhani nchini Oman, Tehran na Muscat zilisaini pia kupitia mawaziri husika wa nchi mbili hati mbili za maelewano ya ushirikiano katika sekta ya kazi na ajira na kustawisha mafunzo ya amali na ya kitaalamu na vilevile juu ya usafirishaji wa nishati ya gesi kutoka Hormozgan kusini mwa Iran kuelekea nchini Oman. Kwa mujibu wa hati hiyo ya maelewano imepangwa kwamba kila mwaka gesi ya ujazo wa mitamchemraba bilioni kumi itasafirishwa kuelekea eneo la Sahar nchini Oman. Mbali na Oman, gesi hiyo itaweza kuuzwa pia kwa nchi nyengine jirani kupitia shirika la pamoja la Iran na Oman.
Baada ya kukamilisha safari yake ya siku mbili nchini Oman Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alirejea nchini hapo jana katika hali ambayo juhudi za kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande mbili na wa kieneo kati ya Iran na Oman umezifanya nchi hizo kuwa washirika wa uhakika na wa kuaminika katika nyuga mbalimbali za kisiasa na kiuchumi
No comments:
Post a Comment