Pages

Saturday, April 26, 2014

Bunge la Burundi launda kamati ya ukweli na maridhiano

Bunge la Burundi launda kamati ya ukweli na maridhiano
Bunge la taifa nchini Burundi limepasishwa muswada wa sheria kuhusiana na kuundwa kamati ya ukweli na maridhiano ya kitaifa nchini humo.
Muswada huo umekuja baada ya kupita miaka 21 tangu taifa hilo likumbwe na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Mwandishi wa Radio Tehran ametuandalia ripoti ifuatayo:WWW:http://kiswahili.irib.ir/habari/mahojiano/item/39735-bunge-la-burundi-launda-kamati-ya-ukweli-na-maridhiano

Prof. Lipumba afafanua kuhusu kundi la UKAWA na malengo yake

Prof. Lipumba afafanua kuhusu kundi la UKAWA na malengo yake
Mwenyekiti Taifa wa chama cha upinzani cha CUF nchini Tanzania, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, amesema kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) litaendelea kupigania haki ya Watanzania ya kupata katiba wanayoitaka na inayoakisi maoni yao waliyoyatoa mbele ya Tume ya Marekebisho ya Katiba. Kundi hilo linajumuisha wajumbe wa bunge maalumu la katiba wanaopinga kile wanachodai ni ubabe wa chama tawala CCM kwenye bunge hilo. Kundi hilo liliondoka bungeni wiki iliyopita likissema kuwa limechoshwa na kusikiliza matusi, na lugha za kejeli na kibaguzi kutoka kwa wajumbe wa CCM na kulalamikia kuburuzwa na chama hicho tawala katika kujadili rasimu ya Katiba mpya.
Salim Swaleh amepata fursa ya kuzungumza na Prof. Lipumba ambaye anajibu baadhi ya maswali muhimu ambayo Watanzania wengi wamekuwa wakijiuliza. Bofya hapa kusikiliza mahojiano hayo au tumia Player iliyopo hapa chini.http://kiswahili.irib.ir/habari/mahojiano/item/39766-prof-lipumba-afafanua-kuhusu-kundi-la-ukawa-na-malengo-yake

Viongozi Nigeria wataka umoja dhidi ya Boko Haram

Viongozi Nigeria wataka umoja dhidi ya Boko Haram
Wakuu wa majimbo ya Nigeria wametaka kuundwa mirengo ya umoja katika kukabiliana na kundi la Boko Haramu na mashambulizi dhidi ya Waislamu na Wakristo nchini humo. Siku ya Alkhamisi Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria aliitisha kikao cha usalama, kwa lengo la kujadili njia za kumaliza mashambulizi ya miaka mitano ya kundi hilo, kikao ambacho kilihudhuriwa na wakuu wa majimbo 36 ya nchi hiyo kutoka pande zote mbili za kusini, eneo lenye wafuasi wengi wa Kikristo na lile la kaskazini ambalo lina Waislamu wengi. Baada ya kikao hicho viongozi hao walitangaza kwa pamoja kuwa, mashambulizi yanayofanywa na kundi la Boko Haram nchini Nigeria si vita vya kidini na kwamba wahanga wa mashambulizi ya kundi hilo ni Waislamu na Wakristo kwa pamoja. Walisisitiza kuwa, mashambulizi ya wanamgambo wa kundi hilo hayatofautishi baina ya Muislamu au Mkristo na hivyo kulitaja kundi la Boko Haram kuwa ni kundi la uhalifu tu.

Ikhwan wahamishwa Qatar na kupelekwa nchini Libya


Ikhwan wahamishwa Qatar na kupelekwa nchini Libya
Duru za habari zimewanukuu maafisa wa Libya kuwa, viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini Misri waliokuwa wakiishi nchini Qatar wamehamishiwa nchini Libya kwa siri. Vyanzo vya habari katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Tripoli vimeeleza kuwa, katika siku za hivi karibuni kumekuwa kukishuhudiwa harakati za kutia shaka sambamba na kuongezeka idadi kubwa ya safari za ndege za kijeshi zinazoingia na kutoka katika uwanja huo. Chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutaja jina lake kimewanukuu baadhi ya maafisa wa serikali nchini Libya wakisema kuwa, ndege hizo zilikuwa zimewabeba viongozi wa harakati ya Ikwanul Muslimin kutoka Qatar, baada ya serikali ya Doha kuamua kuwahamisha kwa siri viongozi hao kuelekea Libya. Kwa mujibu wa chanzo hicho, Sheikh Yusuf Qardhawi, Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Maulama wa Kiislamu karibuni hivi atapelekwa nchini Tunisia. Inaelezwa kuwa, uhamishaji huo wa viongozi wa harakati ya Ikwanul Muslimin kutoka Doha kwenda Tripoli, kunafanyika chini ya usimamizi wa vyombo vya usalama na intelijensia vya Qatar. Kwa mujibu wa makubaliano ya hivi karibuni yaliyotiwa saini mjini Riyadh Saudia, Qatar inatakiwa kuangalia upya siasa zake sambamba na kuacha kuiunga mkono harakati ya Ikwanul Muslimin ya nchini Misri. Inaelezwa kuwa, miezi miwili iliyopita Saudi Arabia, Imarati na Bahrain ziliondoa mabalozi wake mjini Doha, Qatar, katika kulalamikia siasa za nchi hiyo za kuendelea kuwaunga mkono wanachama wa Ikwanul Muslimin. Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, alikadhibisha taarifa iliyosambazwa na vyombo vya habari kuhusiana na kuhamishiwa nchini humo ofisi ya Sheikh Yusuf Qardhawi na kusema kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote.

Saudia na Ufaransa zataka kuharibu uchaguzi wa Syria

Saudia na Ufaransa zataka kuharibu uchaguzi wa Syria
Saudia na Ufaransa nchi mbili zinazounga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria, zinafanya njama za kuvuruga uchaguzi wa nchi hiyo. Habari zinaeleza kuwa, viongozi wa nchi hizo mbili wamekuwa wakifanya mazungumzo katika eneo la karibu na mpaka wa Jordan na Syria ili kuhakikisha zinazuia kufanyika uchaguzi mkuu wa Syria. Gazeti la 'Al-Manar' la Palestina limeandika kuwa, Saudia na Ufaransa zimepatwa na wahka mkubwa kufuatia ushindi mkubwa wa jeshi la Syria dhidi ya makundi ya kigaidi katika maeneo ya mji wa Homs sambamba na kufunga njia za kupitishia misaada kuelekea kwa makundi hayo ya kigaidi katika miji ya Aleppo, huko kaskazini mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Riyadh na Paris hivi sasa zinayashawishi makundi ya kigaidi kufungua maeneo ya Homs ambayo sasa yanadhibitiwa na jeshi la serikali. Gazeti la 'Al-Manar' limeongeza kuwa, Saudia na Ufaransa zinafanya njama za kuyapatia makundi ya kigaidi makombora ya kutungulia ndege nchini humo. Hivi karibuni Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria alitangaza kuwa, tayari nchi hiyo imeshachukua hatua madhubuti za kuhakikisha kuwa uchaguzi wa rais unafanyika kwa salama na kuongeza kuwa, hata hivyo maadui wa taifa na wananchi wa Syria wanafanya njama ili kuzuia tukio hilo la kihistoria lisifanyike nchini humo.

Kenya yataka kukomeshwa mapigano nchini S/Kusini

Kenya yataka kukomeshwa mapigano nchini S/Kusini
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametaka kurejeshwa hali ya usalama na amani nchini Sudan Kusini. Rais Kenyatta amezitaka pande hasimu zinazoongoza mapigano nchini Sudan Kusini kuhakikisha zinakomesha vita vya ndani haraka iwezekanavyo. Hadi hivi sasa vita hivyo vimeshapelekea maelfu ya raia kuuawa. Aidha Rais Kenyatta ameonya kuwa nchi za eneo hilo la Afrika hazitaruhusu kutokea maafa mengine kwa wananchi wa taifa lolote la bara la Afrika. Mapigano nchini Sudan Kusini yaliibuka mwezi Disemba mwaka jana baada ya kufeli jaribio la kutaka kuiangusha serikali ya Rais Salva Kiir. Zaidi ya watu 1000 wameuawa na wengine laki tisa kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Wakati huo huo na katika juhudi za kurejesha maridhiano kati ya wananchi wa taifa hilo, mahakama moja nchini Sudan Kusini imewaachilia huru viongozi wanne wlioasi ambao walikuwa wakituhumiwa kufanya uhaini na njama za kutaka kuiangusha serikali kuu ya Juba. Hatua hiyo, imefanyika katika hali ambayo viongozi wa pande mbili wanaohusika katika mgogoro wa nchi hiyo, wanakabiliwa na tishio la kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa kutokana na kuendeleza mauaji na ukatili katika taifa hilo.

UN:Kuwahamisha kwa nguvu Waislamu CAR

UN: Haifai kuwahamisha kwa nguvu Waislamu CAR
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, haifai kuwalazimisha Waislamu waache nchi yao ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuwapeleka nje ya nchi hiyo bila ya ridhaa yao. Hayo yamesemwa na maripota wawili maalumu wa haki za wakimbizi wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao ni Chaloka Beyani, na Rita Izsák na kusisitiza kuwa, kuwahamisha nje ya nchi wakimbizi lazima kuzingatie sheria hasa pale inapotokea maisha ya wakimbizi hao kuwa hatarini. Maripota hao wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, ikiwa hatua hiyo itatekelezwa bila kufuata sheria, basi itahesabika kuwa ni kujichukulia hatua mkononi. Maafisa hao maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesisitiza kuwa, kuna udharura wa kuwapa fursa ya kuchagua Waislamu nchini humo kati ya kubakia au kuondoka nje ya nchi na kurejea makwao baada ya kupatikana hali ya usalama na amani nchini humo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, walilaani hatua ya askari wa Ufaransa kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), ya kuwahamisha kiholela Waislamu wa nchi hiyo na kuwapeleka katika maeneo yasiyo rasmi au nje ya nchi hiyo, na kuongeza kuwa, hatua hiyo itaharibu umoja wa kitaifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.