Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Tisa Jamadut-Thani 1435 Hijria sawa na tarehe 26 Aprili mwaka 2014 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita yaani tarehe 26 Aprili mwaka 1964, nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kabla hapo Tanganyika na Zanzibar zilikuwa chini ya tawala mbalimbali ambapo mtawala wa mwisho alikuwa Muingereza. Tanganyika ilijikomboa na kupata uhuru mwaka 1961 na Zanzibari kwa upande wake ilipata uhuru mwaka 1963. Mnamo mwaka 1964, Julius Kambarage Nyerere Rais wa wakati huo wa Tanganyika alitaka kuweko muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ambapo katika tarehe kama ya leo lengo hilo lilitimia. Kijiografia Tanzania iko mashariki mwa Afrika ikiwa inapakana na Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji.
***
Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl huko Ukraine ambacho kilikuwa kikidhamini sehemu kubwa ya nishati ya umeme ya nchi hiyo kiliripuka na kusambaza mada hatari za miale ya nunurishi au radioactive. Awali Umoja wa Kisovieti ulikadhibisha habari ya kutokea mlipuko katika kituo hicho. Hata hivyo baadaye ulilazimika kukiri kutokea mlipuko huo baada ya kuenea mada za nunurishi kutokea katika kituo hicho. Kasoro za kiufundi zilitajwa kuwa chanzo cha mlipuko huo. Mwaka 2000 Ukraine ilikifunga kabisa kituo cha nyuklia cha Chernobyl.
***
Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Kuogofya la Gestapo la Ujerumani liliasisiwa. Shirika hilo liliasisiwa na Hermann Wilhelm Goering aliyekuwa mmoja wa maafisa wa juu wa Adolph Hitler kiongozi wa Wanazi wa Ujerumani. Shirika hilo lilikuwa ni polisi wa siri wa Kijerumani katika kipindi cha utawala wa Wanazi. Jukumu la German for Secret State Police, kama lilivyojulikaa pia, lilikuwa ni kuwafatilia, kuwatia mbaroni na kuwanyongwa watu waliokuwa wakimpinga Hitler na siasa zake za Kinazi. Kiongozi mashuhuri kabisa wa Gestapo alijulikana kwa jina la Heinrich Himmler na alianza kuwaongoza polisi hao wa siri wa Kijerumani mwaka 1934.
Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita mwafaka na tarehe 26 Aprili mwaka 1996, mashambulizi ya kijeshi yaliyodumu kwa siku 16 ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon yaliyojulikana kwa jina la "Vishada vya Hasira" yalimalizika. Katika operesheni hiyo, jeshi la Israel lilifanya mashambulio ya nchi kavu, anga na baharini huko kusini na hata katika ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Mbali na kuharibu maeneo mengi ya raia na miundo mbinu na taasisi za kiuchumi, utawala haramu wa Israel uliwaua shahidi raia 180 wa Lebanon na kujeruhi mamia ya wengine.
***
Na siku kama ya leo miaka 1427 kulingana na kalenda ya Hijria, vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (s.a.w), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waenda kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye huyo pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (a.s) kwa umahiri mkubwa aliwashambulia maadui na kurejea Madina na ushindi.
***
No comments:
Post a Comment