Duru za habari zimewanukuu maafisa wa Libya kuwa, viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini Misri waliokuwa wakiishi nchini Qatar wamehamishiwa nchini Libya kwa siri. Vyanzo vya habari katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Tripoli vimeeleza kuwa, katika siku za hivi karibuni kumekuwa kukishuhudiwa harakati za kutia shaka sambamba na kuongezeka idadi kubwa ya safari za ndege za kijeshi zinazoingia na kutoka katika uwanja huo. Chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutaja jina lake kimewanukuu baadhi ya maafisa wa serikali nchini Libya wakisema kuwa, ndege hizo zilikuwa zimewabeba viongozi wa harakati ya Ikwanul Muslimin kutoka Qatar, baada ya serikali ya Doha kuamua kuwahamisha kwa siri viongozi hao kuelekea Libya. Kwa mujibu wa chanzo hicho, Sheikh Yusuf Qardhawi, Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Maulama wa Kiislamu karibuni hivi atapelekwa nchini Tunisia. Inaelezwa kuwa, uhamishaji huo wa viongozi wa harakati ya Ikwanul Muslimin kutoka Doha kwenda Tripoli, kunafanyika chini ya usimamizi wa vyombo vya usalama na intelijensia vya Qatar. Kwa mujibu wa makubaliano ya hivi karibuni yaliyotiwa saini mjini Riyadh Saudia, Qatar inatakiwa kuangalia upya siasa zake sambamba na kuacha kuiunga mkono harakati ya Ikwanul Muslimin ya nchini Misri. Inaelezwa kuwa, miezi miwili iliyopita Saudi Arabia, Imarati na Bahrain ziliondoa mabalozi wake mjini Doha, Qatar, katika kulalamikia siasa za nchi hiyo za kuendelea kuwaunga mkono wanachama wa Ikwanul Muslimin. Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, alikadhibisha taarifa iliyosambazwa na vyombo vya habari kuhusiana na kuhamishiwa nchini humo ofisi ya Sheikh Yusuf Qardhawi na kusema kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote.
No comments:
Post a Comment