Pages

Saturday, April 26, 2014

Kenya yataka kukomeshwa mapigano nchini S/Kusini

Kenya yataka kukomeshwa mapigano nchini S/Kusini
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametaka kurejeshwa hali ya usalama na amani nchini Sudan Kusini. Rais Kenyatta amezitaka pande hasimu zinazoongoza mapigano nchini Sudan Kusini kuhakikisha zinakomesha vita vya ndani haraka iwezekanavyo. Hadi hivi sasa vita hivyo vimeshapelekea maelfu ya raia kuuawa. Aidha Rais Kenyatta ameonya kuwa nchi za eneo hilo la Afrika hazitaruhusu kutokea maafa mengine kwa wananchi wa taifa lolote la bara la Afrika. Mapigano nchini Sudan Kusini yaliibuka mwezi Disemba mwaka jana baada ya kufeli jaribio la kutaka kuiangusha serikali ya Rais Salva Kiir. Zaidi ya watu 1000 wameuawa na wengine laki tisa kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Wakati huo huo na katika juhudi za kurejesha maridhiano kati ya wananchi wa taifa hilo, mahakama moja nchini Sudan Kusini imewaachilia huru viongozi wanne wlioasi ambao walikuwa wakituhumiwa kufanya uhaini na njama za kutaka kuiangusha serikali kuu ya Juba. Hatua hiyo, imefanyika katika hali ambayo viongozi wa pande mbili wanaohusika katika mgogoro wa nchi hiyo, wanakabiliwa na tishio la kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa kutokana na kuendeleza mauaji na ukatili katika taifa hilo.

No comments:

Post a Comment