Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesema kuwa, bara la Afrika linatakiwa kujifunza jambo kutokana na mafanikio yaliyopatikana kupitia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 50 sasa. Rais Kikwete amesema kuwa, kudumu kwa muungano huo na kuendelea kuimarika kwa nusu karne, sio jambo linalofaa kubezwa na nchi yoyote kwa kuwa zipo baadhi ya nchi zilizojaribu kufanya hivyo, lakini hazikufanikiwa. Rais Jakaya Kikwete aliyasema hayo hapo jana jijini Dar es Salaam, Tanzania, kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wakati akipokea matembezi ya vijana na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari. Alisema kama ninavyomnukuu, “Wapo wenzetu barani Afrika waliojaribu, lakini hawakufanikiwa kama sisi, kwani muungano wao ulidumu muda mfupi na kusambaratika. Wapo waliokaa miaka miwili, miezi na wapo ambao wameanza majadiliano mpaka leo hawajamaliza.” Mwisho wa kunukuu. Aidha Rais Kikwete alinukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere, kwa kusema kama ninavyomnukuu: “Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika, nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka ukoloni, Tanzani ni ya kuundwa na sisi wenyewe.” Mwisho wa kunukuu.
No comments:
Post a Comment