Pages

Saturday, April 26, 2014

Mauaji ya waandishi wa habari yameongezeka duniani


Mauaji ya waandishi wa habari yameongezeka duniani
Kituo cha uhuru wa vyombo vya habari nchini Sudan, kimetangaza kuongezeka mauaji dhidi ya waandishi wa habari duniani. Kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya kituo hicho, waandishi wa habari 172 wameuawa mwaka jana katika nchi 26 duniani kiwango ambacho ni zaidi ya kile cha mwaka juzi 2012. Aidha ripoti ya kituo hicho cha uhuru wa vyombo vya habari nchini Sudan imeeleza kuwa,  mwaka 2012 waandishi wa habari 140 waliuawa katika nchi 28. Ripoti hiyo imeongeza kwamba, mbali na mauaji kutiwa mbaroni, kupandishwa kizimbani, kutishiwa usalama na kufanyiwa miamala mibaya waandishi wa habari, lakini wahusika wake hawatiwi mbaroni. Kituo hicho kimeitaja Uturuki kuwa nchi ya kwanza kwa vitendo hivyo, ambapo waandishi wa habari 40 walitiwa mbaroni mwaka 2012 pekee nchini humo. Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Press Emblem Campaign (PEC), Blaise Lempen alinukuliwa akisema kuwa, kuna haja kwa kila nchi kufanyia kazi azimio la tarehe 28 mwezi Machi mwaka huu la Baraza la Haki za Binaadamu juu ya udharura wa  kulindwa waandishi wa habari wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Al Maliki apinga njama za kutaka kuigawa Iraq

  • Al Maliki apinga njama za kutaka kuigawa Iraq
Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al Maliki amepinga vikali njama za kutaka kuigawa nchi hiyo na kuakhirishwa uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanyika hivi karibuni nchini humo.
Nouri al Maliki amesema kuwa, baadhi ya watu wanafanya njama za kuigawa nchi hiyo na kusisitiza kwamba eneo la Kurdistan au maeneo mengine yoyote ya nchi hiyo, hayana haki ya kujitenga na serikali kuu ya nchi hiyo. Waziri Mkuu wa Iraq ameongeza kuwa, takwa kama hilo linakinzana kikamilifu na Katiba ya Iraq ambayo inasisitiza juu ya kuwepo umoja na mshikamano wa kitaifa. Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, hakuna mivutano kati ya madhehebu za kidini nchini humo bali makundi ya kisiasa ndiyo yanayofanya juhudi za kupata uungaji mkono kutoka kwa wananchi kwenye kinyang'anyiro hicho cha uchaguzi wa bunge.
Wakati huohuo, Udey al Khadran, Mkuu wa wilaya ya Khales katika jimbo la Diyala mashariki mwa Iraq amesema kuwa, Qatar na Saudi Arabia zinawaunga mkono kifedha baadhi ya wagombea ambao  mara kwa mara wamekuwa wakifanya njama za kuzusha fitina, umwagaji damu na machafuko nchini humo. Uchaguzi wa Bunge la Iraq umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili.

Abdoulaye Wade arejea nchini Senegal

Abdoulaye Wade arejea nchini Senegal
Rais wa zamani wa Senegal, Abdoulaye Wade, amefanikiwa kurejea nchini humo chini ya ulinzi mkali na baada ya kuishi uhamishoni kwa miaka miwili. Wade mwenye umri wa miaka 87 aliyekuwa madarakani tangu mwaka 2000 hadi 2012 baada ya kushindwa katika uchaguzi na Rais Macky Sall wa nchi hiyo, alielekea nchini Ufaransa na kuishi huko kwa kipindi chote hicho. Inaelezwa kuwa, kurejea kiongozi huyo wa zamani nchini Senegal, ni kutaka kuwa karibu na mwanawe Karim Wade ambaye anaendelea kuzuiliwa katika korokoro ya nchi hiyo kwa tuhuma za ufisadi wa kifedha wa mamilioni ya dola za Kimarekani. Mwana huyo wa Wade amekuwa kizuizini nchini Senegal kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa huku akitazamiwa kupandishwa kizimbani mwezi Juni mwaka huu kwa tuhuma hizo. Karim Wade anadaiwa kutumia njia zisizo halali katika kupata utajiri huo wakati wa utawala wa baba yake Abdoulaye Wade. Wade ameituhumu serikali ya Rais Macky Sall wa nchi hiyo kwa kuzuia makusudi kutolewa idhini ya kutua ndege iliyokuwa imembeba katika uwanja wa ndege wa Dakar na hivyo kulazimika kutua Dar Al-Bayda nchini Morocco hapo siku ya Jumatano iliyopita.

zamani leo -Jumamosi, Aprili 26, 2014


Jumamosi, Aprili 26, 2014
Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Tisa Jamadut-Thani 1435 Hijria sawa na tarehe 26 Aprili mwaka 2014 Miladia.

Siku kama  ya leo miaka 50 iliyopita yaani tarehe 26 Aprili mwaka 1964, nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kabla hapo Tanganyika na Zanzibar zilikuwa chini ya tawala mbalimbali ambapo mtawala wa mwisho alikuwa Muingereza. Tanganyika ilijikomboa na kupata uhuru mwaka 1961 na Zanzibari kwa upande wake ilipata uhuru mwaka 1963. Mnamo mwaka 1964, Julius Kambarage Nyerere Rais wa wakati huo wa Tanganyika alitaka kuweko muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ambapo katika tarehe kama ya leo lengo hilo lilitimia. Kijiografia Tanzania iko mashariki mwa Afrika ikiwa inapakana na Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji.
***
Katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl huko Ukraine ambacho kilikuwa kikidhamini sehemu kubwa ya nishati ya umeme ya nchi hiyo kiliripuka na kusambaza mada hatari za miale ya nunurishi au radioactive. Awali Umoja wa Kisovieti ulikadhibisha habari ya kutokea mlipuko katika kituo hicho. Hata hivyo baadaye ulilazimika kukiri kutokea mlipuko huo baada ya kuenea mada za nunurishi kutokea  katika kituo hicho. Kasoro za kiufundi zilitajwa kuwa chanzo cha mlipuko huo. Mwaka 2000 Ukraine ilikifunga kabisa kituo cha nyuklia cha Chernobyl.
***
Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Kuogofya la Gestapo la  Ujerumani liliasisiwa. Shirika hilo liliasisiwa na Hermann Wilhelm Goering aliyekuwa mmoja wa maafisa wa juu wa Adolph Hitler kiongozi wa Wanazi wa Ujerumani. Shirika hilo lilikuwa ni polisi wa siri wa Kijerumani katika kipindi cha utawala wa Wanazi. Jukumu la German for Secret State Police, kama lilivyojulikaa pia, lilikuwa ni kuwafatilia, kuwatia mbaroni na kuwanyongwa watu waliokuwa wakimpinga Hitler na siasa zake za Kinazi. Kiongozi mashuhuri kabisa wa Gestapo alijulikana kwa jina la Heinrich Himmler na alianza kuwaongoza polisi hao wa siri wa Kijerumani mwaka 1934.
Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita mwafaka na tarehe 26 Aprili mwaka 1996, mashambulizi ya kijeshi yaliyodumu kwa siku 16 ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon yaliyojulikana kwa jina la "Vishada vya Hasira" yalimalizika. Katika operesheni hiyo, jeshi la Israel lilifanya mashambulio ya nchi kavu, anga na baharini huko kusini na hata katika ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Mbali na kuharibu maeneo mengi ya raia na miundo mbinu na taasisi za kiuchumi, utawala haramu wa Israel uliwaua shahidi raia 180 wa Lebanon na kujeruhi mamia ya wengine.
***
Na siku kama ya leo miaka 1427 kulingana na kalenda ya Hijria, vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (s.a.w), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waenda kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye huyo pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (a.s) kwa umahiri mkubwa aliwashambulia maadui na kurejea Madina na ushindi.
***

JK: Muungano wa Tanzania ni kigezo kwa Afrika

Rais Jakaya Kikwete wa TanzaniaRais Jakaya Kikwete wa Tanzania

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesema kuwa, bara la Afrika linatakiwa kujifunza jambo kutokana na mafanikio yaliyopatikana kupitia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 50 sasa. Rais Kikwete amesema kuwa, kudumu kwa muungano huo na kuendelea kuimarika kwa nusu karne, sio jambo linalofaa kubezwa na nchi yoyote kwa kuwa zipo baadhi ya nchi zilizojaribu kufanya hivyo, lakini hazikufanikiwa. Rais Jakaya Kikwete aliyasema hayo hapo jana jijini Dar es Salaam, Tanzania, kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wakati akipokea matembezi ya vijana na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari. Alisema kama ninavyomnukuu, “Wapo wenzetu barani Afrika waliojaribu, lakini hawakufanikiwa kama sisi, kwani muungano wao ulidumu muda mfupi na kusambaratika. Wapo waliokaa miaka miwili, miezi na wapo ambao wameanza majadiliano mpaka leo hawajamaliza.” Mwisho wa kunukuu. Aidha Rais Kikwete alinukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere, kwa kusema kama ninavyomnukuu: “Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika, nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka ukoloni, Tanzani ni ya kuundwa na sisi wenyewe.” Mwisho wa kunukuu.

Bunge la Somalia kujadili sheria ya ugaidi

Wabunge wa Somalia wakiwa kwenye vikao vya bungeWabunge wa Somalia wakiwa kwenye vikao vya bunge
Serikali ya Somalia imewasilisha bungeni muswada wa kukabiliana na ugaidi nchini humo. Waziri Mkuu Abdiweli Sheikh Ahmed wa Somalia ameonyesha matarajio yake kwamba, sheria ya kukabiliana na ugaidi inayotarajiwa kupasishwa na bunge la nchi hiyo itaiwezesha serikali yake kuyaadhibu makundi ambayo yanaendesha harakati za kigaidi katika ardhi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, muswada huo unatazamiwa kujadiliwa na bunge la nchi hiyo wiki zijazo. Somalia imekuwa ikikabilia na wimbi la mashambulizi ya wanamgambo wa kundi la ash-Shabab ambapo hivi karibuni watu wasiojulikana walimpiga risasi na kumuua mbunge mmoja katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu, akiwa ni mbunge wa pili wa Bunge la nchi hiyo kuuawa katika kipindi kisichopungua masaa 24. Vikosi vya Jeshi la Somalia vikishirikiana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM vinatekeleza operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa ash-Shabab.

Watuhumiwa wa uhaini wapandishwa kizimbani Rwanda

Watuhumiwa wa uhaini wapandishwa kizimbani Rwanda
Washukiwa wanne wa uhaini waliokamatwa wiki iliyopita nchini Rwanda wamefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Jumatatu hii. Baadhi ya watuhumiwa wamekiri kuhusika kwenye njama za kutaka kufanya mauaji dhidi ya viongozi wa serikali akiwemo Rais Paul Kagame.

Sauti na Video